Ijumaa 7 Novemba 2025 - 11:16
Ulimi; Chombo Kwa Ajili ya Ukombozi au Maangamizi!!

Hawza/ Ulimi ni kiungo kidogo lakini chenye umuhimu mkubwa mno; kwani unapotoka kutoka katika udhibiti wa akili, hauishii tu kumdhalilisha mtu kimaadili, bali pia huufanya moyo wake kuwa mgumu na wenye giza. Amiri al-Mu’minin (a.s.) anaonya akisema: “Yeyote atakayeupa ulimi wake mamlaka juu yake, atadhalilika.”

Shirika la Habari la Hawza — Amiri al-Mu’minin (a.s.) katika Nahjul-Balaghah kuhusiana na umuhimu wa kuudhibiti ulimi amesema:

«هَانَتْ عَلَیْهِ نَفْسُهُ مَنْ أَمَّرَ عَلَیْهَا لِسَانَه.»

“Yeyote anayeupa ulimi wake mamlaka juu yake, atakuwa amejidhalilisha.” [1]

Sherehe:
Viungo vyote katika mwili wa mwanadamu vinapaswa kuwa chini ya utawala wa akili. Iwapo kiungo chochote kitaacha kuwa chini ya udhibiti wa akili, madhara makubwa ya kidunia na ya kiakhera yatampata mtu huyo.

Miongoni mwa viungo vyote, kilicho katika hatari kubwa zaidi ya kupotoka ni ulimi — kiungo ambacho kinapojitenga kutoka kwenye udhibiti wa akili, huharibu maadili na thamani za kiroho kwa kiwango kikubwa.

Imam Sajjad (a.s.) katika hadithi akielezea hali ya ulimi amesema:

«إِنَّ لِسَانَ اِبْنِ آدَمَ یُشْرِفُ کُلَّ یَوْمٍ عَلَی جَوَارِحِهِ فَیَقُولُ کَیْفَ أَصْبَحْتُمْ؟ فَیَقُولُونَ بِخَیْرٍ إِنْ تَرَکْتَنَا، وَیَقُولُونَ اَللَّهَ اَللَّهَ فِینَا، وَیُنَاشِدُونَهُ، وَیَقُولُونَ إِنَّمَا نُثَابُ بِکَ وَنُعَاقَبُ بِکَ.» [2]

“Ulimi wa mwanadamu kila siku huvisogelea viungo vyake na kuviuliza: Mmeamkaje? Navyo hujibu: Tuko salama endapo utatuacha tutulie. Kisha humwambia: Mche Mungu kuhusu sisi, usituingize kwenye maovu, tunaapa kwa jina la Mungu; kwani sisi tunapata thawabu kwa sababu yako, na tunapata adhabu kwa sababu yako.”

Hivyo basi, onyo la Amiri al-Mu’minin (a.s.) kuhusu utawala wa ulimi linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Ulimi unapaswa kushikwa kwa hatamu za akili na kutumika katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwani ukitumiwa nje ya njia ya Mwenyezi Mungu, hauleti uharibifu kwa mwenyewe tu, bali pia huathiri viungo vingine kwa ugumu na giza la moyo.

Nabii Isa (a.s.) amesema kuhusu hili:


«لا تُکثِرُوا الکَلامَ فی غَیرِ ذِکرِ اللهِ؛ فإنَّ الَّذینَ یُکثِرُونَ الکلامَ فی غَیرِ ذِکرِ اللهِ قاسِیَةٌ قُلُوبُهُم وَلکِن لا یَعلَمُونَ.» [3]

“Msikithirishe maneno yasiyo ya kumtaja Mwenyezi Mungu; kwa kuwa wale wanaozungumza sana bila kumtaja Mwenyezi Mungu, mioyo yao huwa migumu, hali wao hawajui.”

Kwa hivyo, mtu anapaswa kuwa mmiliki wa ulimi wake, ili kama alivyoeleza Amiri al-Mu’minin (a.s.), asije akajutia matendo yake:

«اِعلَمُوا اَیُّهَا النَّاسُ اَنَّهُ مَن لَم یَملِکُ لِسانَهُ، یَندَم.» [4]

“Enyi watu! Fahamuni kwamba yeyote asiyeudhibiti ulimi wake, bila shaka atajutia.”

Rejea:
1. Nahjul-Balaghah, hekima ya 2.
2. Khisaal, juzuu ya 1, uk. 5.
3. Al-Kafi, juzuu ya 2, uk. 114.
4. Bihar al-Anwar, juzuu ya 74, uk. 280.

Imetayarishwa na Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha